WATU sita wamekufa na wengine 38 kujeruhiwa , baada ya basi lenye namba za usajili T 798 AKV mali ya Lupondije Express kutoka Mwanza kwenda Iringa, kupinduka kwenye mteremko wa mlima Ipogolo mjini Iringa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alisema basi hilo lilipata ajali juzi saa 3:30 usiku wakati likienda Stendi ya Ipogolo, kufaulisha abiria waliokuwa wakienda mkoani Mbeya.
Imeelezwa kuwa baadhi ya abiria waliokufa na majeruhi ni ambao walitakiwa kushuka stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani mjini Iringa lakini hawakushwa kwa kile kilichoelezwa dereva wa basi hilo alikuwa akitaka kuwawahisha abiria wa kwenda Mbeya katika basi lingine lililokuwa likiwasubiri stendi ya Ipogolo.
Kamanda Kakamba alisema basi hilo lilimshinda dereva, Castory Mwalusako (35) wakati akiteremka mlima kutokana na kupoteza upepo kwenye breki, ndipo lilipoteza mwelekeo na kupinduka. Dereva huyo alikimbia lakini polisi walifanikiwa kumkamata.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim alisema walipokea miili ya watu wanne waliofia katika ajali hiyo na wengine wawili walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitalini hapo. Dk Salim alisema waliokufa ni wanaume wanne na wanawake wawili.
Waliotambulika ni Makka Msigwa na Venant Mhagama aliyefia wadini. Alisema majeruhi 38 walifikishwa Hospitali ya Mkoa ya Iringana 11 kati yao walitibiwa na kuruhusiwa. Wengine 27 wamelazwa huku baadhi yao wakiwa mahututi.
Kamanda wa Polisi aliwataja majeruhi ni Banenda Helen (45) raia wa Kongo, Mbuyi Leoni (52) raia wa Kongo, Jojina Nyamboko (26) mkazi wa Songea, Magambo Masunga (51) mkazi wa Mwanza, Felister Mwinuka (19) mkazi wa Njombe, Tubilisiusy Selestine (33), Said Kitonyi (17), Richard Bett (33) raia wa Kenya na Jofa Abonga (30) mkazi wa Geita.
Wengine ni Victor Lameck (25) mkazi wa Kagera, Pius Samwel (20) mkazi wa Mara, Michael Hadu (46) mkazi wa Madaba, Ruvuma, Hassan Mfaume (20) mkazi wa Iringa, Heriet Mwitinda (29) mkazi wa Arusha, Kiliana Kalinga (22) mkazi wa Mbeya, Hima Kifyasi (32) mkazi wa Bariadi, Omary Hassan (35) mkazi wa Makambako, Zuo Pawa (30) mkazi wa Mbeya na Chacha John (26) mkazi wa Iringa.
Majeruhi wengine ni Timoth Sichoni (24) mkazi wa Dodoma, Ishimwe Jasmin (9) rais wa Rwanda, Mkagasana Sarafina (41) rais wa Rwanda, Zaina Kisaka (26) mkazi wa Manyara, Sara Sichone (26) mkazi wa Mwanza, Ivon Magaiwa (22) mkazi wa Mafinga, Solomoni Angolisye (58) mkazi wa Dodoma, Ivan Huwen (33).
Mwingine hajajulikana jina kutokana na kuwa katika hali mbaya. Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, James John alisema walitoka Mwanza vizuri na walipofika Iringa mjini, dereva alikataa kuwashusha abiria waliokuwa wakiishia hapo kwa madai ya kutaka kuwapeleka abiria waliokuwa wakienda Mbeya, wakapakiwe kwenye basi lingine eneo la Ipogolo.
Post A Comment: